Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jana Machi 15, 2022 ilifanya ziara Makao Makuu ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ili kukagua maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa Maabara changamana awamu ya pili.
Katika ziara hiyo Kamati ya bunge iliipongeza TAEC kwa hatua kubwa iliyofikia katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo unajengwa na Serikali kwa jumla ya kiasi cha fedha TZShs Billioni 10.4
Akitoa taarifa ya mradi kwa Kamati ya Bunge Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Profesa Lazaro Busagala alisema awali TAEC iliingia mkataba na Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA) kwa ajili ya ujenzi wa maabara awamu ya kwanza tarehe 29 Mei 2017.
Ujenzi rasmi wa Maabara changamano awamu ya kwanza uliaanza tarehe 01 Juni 2017, ambapo ulikamilika kwa kiasi cha shilingi billion 2.3 na kuzinduliwa rasmi na Mh. Kassim M. Majaliwa (Mb) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 29 Aprili 2018.
Ujenzi wa Maabara ya Awamu ya kwanza ulihusisha Maabara zifuatazo; i. Maabara ya Kupima viasili kwenye sampuli mbalimbali (XRF Laboratory) ii. Maabara ya kupima viwango vya mionzi kwa wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye mazingira yenye mionzi (Person monitoring Dosimetry). iii. Maabara ya uhakiki wa vifaa vya kupimia mionzi (Secondary Standard Dosimetry Lab) iv. Maabara ya kupima vyanzo na kiwango cha mionzi iliyopo kwenye mwili wa binadamu (Whole body counter) v. Kituo cha mafunzo ya ulinzi na usalama wa vyanzo vya mionzi (Nuclear Security Support Center)
Katika taarifa hiyo Profesa Busagala alisema ujenzi wa maabara changamana awamu ya pili TAEC iliingia mkataba na LI JUN DEVELOPMENT CONSTRUCTION CO. LTD tarehe 10 Septemba 2019, ambapo mkataba wa ujenzi wa maabara hiyo ulikuwa ni wa miaka mitatu (3)
Ujenzi rasmi wa Maabara changamano awamu ya pili uliaanza tarehe 23 Septemba 2019, ambapo jiwe la msingi la ujenzi huo liliwekwa rasimi Mhe. Prof Joyce L. Ndalichako (Mb) aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Technolojia tarehe 29 Machi 2020 na Gharama yote ya mradi huo una thamani ya shilingi 10.4 bilioni.
Ujenzi wa Maabara ya Awamu ya pili unahusisha Maabara zifuatazo: i. Maabara ya kupima mionzi ya Alpha (Alpha Spectrometry Laboratory); ii. Maabara ya kupima mionzi ya Beta (Beta Counting Laboratory); ya kupima mionzi ya Gamma (Gamma Spectrometry Laboratory); iii. Maabara ya kupima mionzi kwenye damu (Cytogenetic Laboratory); iv. Maabara ya kupima viwango vya metali kwenye sampuli (X-Ray Fluorescence Laboratory); 4 v. Maabara ya kufanya matengenezo ya vifaa vya mionzi (Nuclear Instrumentation and Maintanance Laboratory); vi. Maabara ya uandaaji wa sampuli kikemikali (Radiochemistry Laboratory); vii. Maabara ya kufanyia matengenezo mabaki ya vyanzo vya mionzi (Radioactive Wastes Conditioning Laboratory).
Profesa Busagala alisema kuwa, hadi kufikia tarehe 09 Machi 2022, hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa maabara changamana awamu ya pili (mradi namba 6352) ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 94 ambapo upo mbele kwa miezi mitatu ukilinganisha na mpango kazi (work program) uliokuwa umepangwa kwenye mkataba.
Akimalizia taarifa yake Profesa Lazaro aliishukuru Kamati ya Bunge na kutoa shukrani za dhati kwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kuisimamia, kuitegemeza na kuiwezesha TAEC katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiiomba Serikali iendelea kuiwezesha Taasisi kufikia malengo yake kwa manufaa ya jamii ya Watanzania