Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) inaendesha mafunzo ya kitaifa kwa wafanyakazi wanaofanya kazi ya kukagua mizigo na bidhaa mbali mbali za wageni wa ndani na nje katika kuzingatia usalama wa mionzi kwenye maeneo yao ya kazi ili kujilinda na kuwalinda Watanzania dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.
Mafunzo haya ya siku tano yalianza jumatatu tarehe 01 Februari 2021, Makao Makuu ya TAEC, Jijini Arusha, ambapo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Dkt Justine Ngaile alifungua mafunzo hayo rasmi na kuwataka washiriki wote kuchukua hatua zote stahiki za kiusalama wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili kuboresha usalama.
Jumla ya maofisa 40 kutoka katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu kama barabara na mamlaka mbalimbali kama vile viwanja vya ndege, hotelini, viwandani na bandarini wanashiriki mafunzo haya ya matumizi salama ya teknolojia ya mionzi kwenye ukaguzi wa mizigo ili kujipatia ujuzi na kuwa bora katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Naamini kozi hii kama inavyojieleza itaweza kuwasaidia katika kujenga ujuzi na ubora katika kuifanya kazi ya ukaguzi wa mionzi kwa usahihi na kuwakinga watanzania dhidi ya mionzi ” Dkt. Ngaile amesema.
Dkt. Ngaile amesema kuwa maofisa hao wana jukumu kubwa katika kuhakikisha wanafanya kazi yao ya ukaguzi kwa kutumia mionzi kwa ueledi ili kuhakikisha usalama kwani vifaa wanavyovitumia kama vile X-Ray ili kugundua aina ya mizigo iliyobebwa ndani kwenye vifungashio ina mionzi mikali, hivyo ni muhimu kuchukua taadhari za kiusalama ili kujilinda wao wenyewe, mazingira, pamoja na wananchi dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mionzi.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Bwana Atumaini Makoba amesema mafunzo ya mwaka huu yamewalenga watendaji wengi zaidi ili kuongeza wigo wa elimu na ushirikiano baina ya watumiaji wa vyanzo vya mionzi na wadhibiti ili kuongeza usalama wa mionzi mahala pa kazi katika kulinda wananchi na mazingira dhidi ya mionzi.