Kozi ya Upimaji wa Vyanzo vya Mionzi Kwenye Maabara za Tume

May 15, 2020

Jumla ya wataalamu nane (8) kutoka mataifa saba (7) ya  nchi za ukanda wa Afrika wamehitimu mafunzo juu ya matumizi sahihi  ya maabara zinazotumia teknolojia ya nyuklia katika udhibiti na uhamasishaji wa matumzi salama wa teknolojia ya nyuklia. Mafunzo haya yaliyofanyika kwa muda wa miezi mitatu Makao Makuu ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, yaliendeshwa na TAEC kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa (EU). 

Katika hafla fupi ya kuhitimisha mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC), Prof. Lazaro Busagala amewataka wahitimu hao kutumia vyema ujuzi walioupata katika kuhakikisha wanawalinda wananchi wao na madhara yatokanayo na mionzi.

“Mmeweza kupata ujuzi wa kutosha katika mafunzo haya hivyo nawaomba mkahakikishe mnatendea haki mlichojifunza na kuelekeza wengine katika nchi zenu” alisema Prof. Busagala.

Aidha, Prof. Busagala ameeleza kuwa pamoja na changamoto ya ungonjwa wa Covid 19 (Korona) ulioathiri Dunia nzima na kusababisha vifo vya maelefu ya watu, bado mafunzo haya yaliweza kuendelea na kumalizika salama. Prof amewasihi wahitimu hao wahakikishe wanachukua tahadhari zote muhimu za kujilinda dhidi ya ugonjwa huu wanapokua wanarejea nchini mwao.

Hata hivyo Prof. Busagala ameuomba umoja wa Ulaya (EU) kuendeleza ushirikiano mkubwa baina yao kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa vifaa vitakavyowekwa kwenye maabara ya awamu ya pili, ambayo alisisitiza kuwa ikikamilika itakuwa ni kituo cha mafunzo ya masuala ya teknlojia ya nyuklia. Ujenzi wa maabara hiyo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2020.

Awali akiwasilisha salamu za  EU, meneja wa mradi Bi Genevieve aliishukuru TAEC kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mafunzo hayo, pamoja kuruhusu wataalamu  wake ambao walishiriki kutoa mafunzo kwa washiriki hao. Bi Genevieve alisistiza kwamba TAEC ni kituo muhimu cha mafunzo ya teknolojia ya nyuklia katika nchi za Afrika Mashiki na kati kwa kuwa imesheheni vifaa vya kisasa vya teknolojia ya nyuklia ambavyo vilitolewa na Jumuiya ya Ulaya (EU).

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo waliishukuru TAEC kwa kukubali kutoa mafunzo hayo na kuwashukuru wakufunzi wote kutoka TAEC na Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kwa utaalamu walioupata huku pia wakiushukuru Umoja wa Ulaya (EU ) kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo.

Hifadhi za nyaraka