KUFUNGIWA KWA HUDUMA YA MIONZI KATIKA VITUO 3 VYA AFYA KANDA YA ZIWA

Nov 12, 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUFUNGIWA KWA HUDUMA YA MIONZI KATIKA VITUO 3 VYA AFYA KANDA YA ZIWA

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) katika ukaguzi wake wa kawaida wa kila mwaka umevifungia vituo vitatu vya afya utoaji wa huduma ya mionzi (X-Ray) kutokana na  kutokidhi matakwa ya Sheria Na. 7 ya Nguvu za Atomiki ya Mwaka 2003 na kwamba vitarejeshewa huduma hiyo mara vituo hivyo vitakaporekebisha mapungufu yaliyoonekana.

Huduma hiyo imefungiwa katika vituo vya afya vifuatavyo:  Hospitali Teule ya Wilaya ya Sumve, Hospitali ya Wilaya ya Ngudu na Hospitali  ya Wilaya ya Misungwi.

Huduma hiyo imefungwa kufuatia ukaguzi unaoendelea kanda ya ziwa ikiwa ni zoezi linalofanyika kila mwaka katika kuhakikisha  usalama wa utoaji wa huduma ya mionzi unafuatwa kama ambavyo  ilivyoelekezwa katika Sheria Na. 7 ya Nguvu za Atomiki Tanzania ya Mwaka 2003 ili kulinda wafanyakazi, wagonjwa, wananchi na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi. Katika  vituo  vya Sumve na Ngudu imegundulika kuwa watumishi wake hawana sifa za upigaji wa picha za mionzi huku katika kituo cha Misungwi imegundulika  kuwa vifaa vyao vya mionzi havina ubora unaostahili.

TAEC inavitaka vituo vyote vinavyotumia mionzi katika utoaji wao wa huduma mbalimbali kuhakikisha vinafuata Sheria na taratibu za  kiusalama kama ilivyoelekzwa katika sheria ikiwemo kuishirikisha TAEC katika hatua zote za ujenzi wa vituo hivyo kwa lengo la kulinda afya za Watanzania.

Katika ukaguzi huu unaoendelea jumla ya vituo 44 vimekaguliwa katika mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza. Kati ya vituo hivyo, vituo  36 ni vya sekta ya afya, vituo viwili (2) ni katika sekta ya migodi, vituo vitatu (3) ni katika sekta ya viwanda, vituo viwili (2) ni  katika sekta ya ujenzi wa barabara na kituo kimoja (1) ni katika sekta ya usafirishaji wa mizigo.