Kuunganisha Mfumo wa Kielektroniki wa Dirisha moja na Mfumo wa Kutoa Vibali vya Mionzi

May 27, 2020

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeendelea na mikakati yake ya kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wote wa ndani na nje ili waweze kufanya biashara bila usumbufu na kulipa kodi stahiki kwa hiari kwa mujibu wa sheria.Moja ya mkakati wake ni kuanzishwa kwa mfumo wa Kielektroniki wa Dirisha Moja la Huduma (Electonic Single Window System) ambao utamuepusha na usumbufu wa kutumia muda mwingi katika kufuatilia vibali vya mzigo na badala yake huduma zote atazipata katika sehemu moja.
Katika hali hiyo basi Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania imeanza kufanya kazi ya kuunganisha katika mfumo wa dirisha moja,  mfumo wake wa vibali na leseni za kuhakiki usalama wa vyakula na vifaa vya vinavyotoa mionzi (https://rac.taec.go.tz/). Kwa sasa wateja hawahitajiki tena kutoka mikoani ili kuleta sampuli za kupimwa katika ofisi za makao makuu ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, kwani maboresho makubwa yamefanyika katika ofisi za kanda na mipakani kwa kuweka vifaa vya kupimia, hivyo mteja atachagua eneo husika analoona ni karibu kwake tofauti na zamani ambapo ilikuwa lazima sampuli zote ziletwe Arusha makao makuu ili kufanyiwa vipimo hivyo.
Matumizi ya Dirisha Moja la Huduma yataboresha huduma kwa wafanyabiashara, ikiwa ni pamoja na kuwaondolea changamoto waliyokuwa wakikutana nayo ya mizigo kukaa muda mrefu bila kushughulikiwa kutokana na kukosa vibali.  Kupitia mfumo huo, wafanyabiashara hawatakuwa wakienda kwenye idara na taasisi za Serikali na badala yake wakiwa kwenye ofisi zao wataweza kuomba na kupata vibali, ikiwa ni pamoja na kupata bili za malipo ambazo watatakiwa kwenda kuzilipia benki au mfumo wa malipo wa serikali kutokana na kuwa mfumo unafanya kazi na benki. Kabla ya mfumo, ili mtu aweze kupata kibali alilzimika kutembelea taasisi husika zaidi ya mara 10 kutokana na kuwa  baadhi ya ofisi hutaka vibali zaidi ya kimoja, lakini kwa kutumia mfumo huo muda utapungua. Ingawa taasisi zinazotoa vibali ni 47, Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ni moja ya  taasisi 32 ambazo kwa pamoja zitaunganishwa awali katika mfumo.

Hifadhi za nyaraka