MAFUNZO YA KITAIFA YA UDHIBITI NA USALAMA WA MIONZI KATIKA IDARA ZA RADIOLOJIA NCHINI

Dec 21, 2019

Arusha, 20 Desemba, 2019
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) leo imefunga rasmi mafunzo ya kitaifa ya siku (5) juu ya udhibiti na usalama wa mionzi katika idara za radiolojia kwa wanaradiolojia 104 (Radiographers) ambao hutumia mionzi kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa kutoka hospitali mbalimbali hapa nchini.
Akifunga rasmi mafunzo hayo yaliyofanyikia Makao Makuu ya Tume hiyo Jijini Arusha leo hii, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Lazaro Busagala, amesema Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wafanyakazi wa hospitali na vituo vya afya kote nchini ili kutoa huduma bora na kuhakikisha huduma za mionzi zinatolewa katika kiwango cha hali ya juu na umakini mkubwa ili kuweza kupunguza uwezekano wa kupata madhara yatokanayo na mionzi endapo sheria na taratibu hazitafuatwa.
Profesa Busagala amesisitiza kuwa usalama dhidi ya mionzi uko mikononi mwa TAEC na watoa huduma wa radiolojia, hivyo sheria, kanuni, taratibu na weredi vitumike ili wagonjwa wanaokwenda kwenye vituo vya afya kupata huduma ya mionzi warudi majumbani mwao wakiwa salama na sio kurudi wakiwa wamepata madhara yaliyosababishwa na mionzi.
Profesa Busagala aliongeza kwa kusema wanaradiolojia ni kiungo muhimu kati ya TAEC na maeneo wanayofanyia kazi hivyo ushirikiano unahitajika zaidi ili kuboresha ustawi wa uchunguzi na utoaji wa huduma ya mionzi .

Imetolewa na;

Peter G. Ngamilo
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania

Hifadhi za nyaraka