Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Profesa Lazaro Busagala akutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Zanzibar Seif Ali Iddi kwenye ofisi yake iliyopo Vuga mjini Unguja siku ya jumatatu tarehe 19/11/2018 alipofika kujitambulisha rasmi.
Profesa Lazaro Busagala amezungumza kwa kina na Makamu wa Rais juu ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kuhusiana na udhibiti na matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia Tanzania Bara na Visiwani katika kuhakikisha wananchi,wafanyakazi na mazingira wanalindwa dhidi ya madhara hatari yanayoweza kusababishwa na mionzi.
Profesa Lazaro amemueleza Makamu wa Pili wa Rais kwamba mpaka sasa kuna jumla ya vituo 700 ambavyo vimekaguliwa, vimesajiliwa na kupewa vibali vya kutoa huduma kwa kutumia vyanzo vya mionzi nchini. Vyanzo hivyo vinajumuisha huduma za Afya, Viwanda, Majenzi, Utafiti, Kilimo na uchenjuaji wa madini.
Prof. Busagala amemwambia Makamu wa Rais juu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya Kilimo kwa kutumia teknolojia ya nyuklia ambapo kutokana na matumizi ya teknolojia hiyo kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji katika kilimo cha Mpunga, Migomba, Mahindi na Shairi hatua iliyoleta matumaini makubwa kwa wakulima hasa upande wa Zanzibar.
Mafanikio hayo yanakwenda sambamba na udhibiti wa maradhi mbali mbali kwenye mimea na Mifugo yaliyokuwa yakisababishwa na wadudu kama Mbung’o ambapo Zanzibar ilifanikiwa kupiga vita maradhi ya ugonjwa wa nagana kufikia mwaka 1998 baada ya upandishaji mbegu za kuzuia ongezeko la Wadudu hao chini ya Utaalamu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA).
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemueleza Mkurugenzi Mkuu na ujumbe wake kwamba jamii bado ina uelewa mdogo juu ya tafsiri sahihi ya masuala ya Nguvu za Atomiki hivyo ipo haja ya wataalamu wa Tume kuendelea kutoa elimu kwa Jamii ili iondoe shaka na ile dhana ya kufikirika kwamba masuala ya atomiki yanatokana na nguvu za kijeshi au mabomu.
Makamu wa Rais alielezea faraja yake kwa kuelewa vizuri majukumu yanayotekelezwa na Tume na kuomba Uongozi wa TAEC kuandaa Mafunzo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaowakilisha Wananchi katika Majimbo yao ili elimu hii iweze kufikishwa kwa Jamii nzima.
Prof. Busagala ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuridhia kutoa eneo la ujenzi wa Maabara kwa upande wa Zanzibar ili Tume iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mzuri na kuimarisha uwezo wa Taifa katika udhibiti na matumizi salama ya mionzi.
Prof. Lazaro S.P. Busagala Kulia akimkabidhi Balozi Seif baadhi ya Vitabu vyenye maelezo ya Majukumu ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania
Angalia mazungumzo kwa njia ya video