Mkutano Wa Kujadili Huduma Ya Matumizi Salama Ya Vyanzo Vya Mionzi Sehemu Za Kazi “ORPAS”

Aug 17, 2022

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu Duniani inafanya kikao cha siku tano ili kujadiliana, kupeana ushauri na kufanya tathmini katika kufata miongozo ya huduma ya matumizi salama ya vyanzo vya mionzi sehemu za kazi

Mkutano huo unafanyika Makao Makuu ya TAEC Jijini Arusha  na jumla ya wataalamu 15 kutoka nchi wanachama wa Shirika la Nguvu za Atomiki wanashiriki zikiwemo Botswana, Burkina Faso, Cameroon, Ghana, Mauritius, Morocco, Namibia, Senegal, Zimbabwe, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (URT) kama nchi mwenyeji na mtaalamu mmoja kutoka Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki.

Lengo kuu la Mkutano huu wa mapitio na Ushauri wa “ORPAS” ni kubaini kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (URT) inafata masharti ya matumizi salama ya mionzi sehemu za kazi kwa kufuata kiwango cha masharti ya kiutendaji ya matumizi salama ya mionzi na kama imeboreshwa kulingana na Mahitaji ya Usalama ya “GSR” Sehemu ya 3 na Mwongozo wa Jumla wa Usalama wa “GSR-7” wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA).

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa Huduma za Teknolojia Na Ufundi Dk.Remigius Kawala alisema “ORPAS ilianzishwa mwaka 2001 ili kuzishauri Nchi Wanachama, pale zitakapoomba, juu ya njia za kuimarisha miundombinu ya kisheria na udhibiti wa matumizi salama ya  mionzi sehemu za kazi, huduma za kiufundi zinazohusiana na usalama wa mionzi, upimaji wa viwango vya mionzi kwa wafanyakazi, uhakiki wa vifaa vya kupimia mionzi; na utekelezaji kwa vitendo wa mpango wa matumizi salama ya  mionzi sehemu za  kazi”.

Dk. Kawala alieleza zaidi kuhusu hitaji la programu za “ORPAS” nchini Tanzania kwani kwa sasa TAEC imetekeleza kwa vitendo programu za matumizi salama ya mionzi sehemu za kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa wafanyakazi katika vituo zaidi ya 1000 vinavyotumia vyanzo vya mionzi  katika  huduma za matibabu, sehemu za viwandani, kwenye ujenzi wa barabara, sekta ya madini n.k ambapo mpaka sasa huduma hii inawanufaisha wafanyakazi 2064 hapa nchini.

Hii ni fursa kwa Tanzania kuwa  mwenyeji wa mkutano wa aina hii  na kufanyika kwa vitendo utoaji wa ushauri kwa nchi wanachama kwa kubadilishana uzoefu uliopatikana katika katika utoaji wa huduma.

Katika siku tano za mkutano, washiriki na wajumbe watakagua na kutathmini utekelezaji wa ORPAS kwa kufanya kazi kwa vitendo katika baadhi ya vituo vilivyochaguliwa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na maabara ya Daraja la pili (Secondary Standard Dosimetry Laboratory-SSDL) katika Makao Makuu ya TAEC, Idara ya Radiolojia katika Hospitali ya NSK na Kampuni ya Bia Tanzania Jijini la Arusha.

Hifadhi za nyaraka