Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo, amepokea Tuzo ya “Plant Mutation Breeding” iliyotolewa kwa mtafiti wa Tanzania, Bwana Salum Faki Hamad, wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI).
Bwana Salum amepewa tuzo hiyo kama utambuzi wa michango yake katika kufanya utafiti wa kutumia teknolojia ya nyuklia katika kuboresha mbegu “Plant Mutation Breeding” na kuibuka kidedea kati ya timu za watafiti 28 kutoka nchi 20.
Tuzo hiyo ilitolewa Septemba 20, 2021 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA), Bwana Rafael Mariano Grossi, katika kikao cha 65 cha Mkutano Mkuu wa IAEA unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Vienna (VIC), Austria.
Bwana Faki alipewa tuzo hiyo baada ya kufanya utafiti ambao ulizaa mbegu ya mpunga ya Supa BC ambayo inazaa zaidi ya asilimia 60 ya mbegu ya asili na inayostahimili ukame na magonjwa mbalimbali.
IAEA, kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), husaidia wataalam ulimwenguni kote kutumia mbinu za nyuklia katika kilimo, pamoja na mbegu zilizonyunyulishwa na mionzi au vifaa vingine vya mmea ili kukuza aina za mimea zilizo na sifa bora.
Utaratibu huu, unaoitwa ufugaji wa mabadiliko ya mimea, hutumia rasilimali asili ya mmea kuiga mchakato wa hiari wa mabadiliko katika uvumbuzi wa mimea. Hii inaongeza kasi ya mabadiliko ya maumbile na inaruhusu wataalamu wa mimea kuchagua zile mbegu zinazohitajika zaidi kutoka katika kundi la mimea iliyonyunyuliswa kwa mionzi.