Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) leo Agosti 22, 2024 katika Makao Makuu ya TAEC Kikombo Dodoma, imefanya semina ya siku moja kwa Waandishi wa Habari wa Jiji la Dodoma ili kutoa elimu juu ya majukumu yanayotekelezwa kisheria na TAEC ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Lengo la semina hii lilikuwa ni kuwapa uelewa wanahabari juu ya majukumu ya kisheria yanayotekelezwa na Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), hasa katika maeneo ya uendelezaji na udhibiti wa matumizi salama ya teknolojia nyuklia na mionzi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akifungua rasmi semina hiyo Mkurugenzi wa sayansi, teknolojia na ubunifu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Ladislaus Mnyone ambaye alikuwa akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, katika hotuba yake aliweka bayana juu ya Majukumu na kazi zinazotekelezwa na TAEC kisheria kwa wanahabari wa Jiji la Dodoma.
Aidha Prof. Mnyone alieleza kuwa TAEC ndio Taasisi pekee iliyopewa mamlaka ya uendelezaji, udhibiti na usimamizi wa matumizi salama ya mionzi hapa nchini, na moja ya majukumu yake makubwa ni kuhakikisha huduma zote zinazotolewa kwa kutumia vyanzo vya mionzi nchini kote, zinatolewa katika usalama wa hali ya juu na umakini mkubwa ili kuweza kupunguza uwezekano wa wananchi na mazingira kupata madhara yanayoweza kusababishwa kutokana na mionzi.
Teknolojia ya nyuklia hutumika katika sekta mbalimbali nchini na duniani kote, ikiwemo afya, elimu, kilimo, mifugo, maji, viwanda, ujenzi, madini, mafuta, gesi pamoja na ukaguzi wa mizigo, na kwa Tanzania hadi sasa kuna jumla ya vituo 1548 katika kipindi cha mwaka 2023/2024 vinavyotumia teknolojia hii “amesema Prof. Mnyone”
Prof. Mnyone aliwashukuru washiriki wa semina kwa kuitikia wito na kutenga muda wao ili kushiriki katika semina hiyo muhimu na kusema kuwa ushiriki wa wanahabari katika semina hiyo utawafanya kuwa mabalozi wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania, katika kutoa elimu kwa umma juu ya kazi mbalimbali zinazofanywa na TAEC, hatimaye kuondoa mtazamo hasi kwa wananchi na wadau wengine waliokuwa wakihusisha utendaji wa TAEC na utengenezaji wa mabomu ya Atomiki.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa Kitengo cha kinga na udhibiti wa mionzi Dkt. Justine Ngaile alipokuwa akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Prof. Najat Kassim Mohammed amesema, TAEC ni Taasisi mtambuka ambapo inafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo uratibu wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika miradi mbalimbali inayotumia teknolojia hiyo wake katika ngazi za kitaasisi na wizara umeksimishwa na unaratibiwa na TAEC.
Katika uratibu huu, mafanikio mbalimbali yamepatikana katika uboreshaji wa matibabu ya saratani katika sekta ya Afya, utafiti wa vyanzo vya maji katika sekta ya Maji, uangalizi wa ubora wa Barabara na majengo katika sekta ya Ujenzi, na sekta nyingine kama vile Nishati, Mifugo, Kilimo, Usafirishaji, Ulinzi n.k. hivyo basi, TAEC ni muhimili wa kusimamia matumizi ya teknolojia hiyo pamoja na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu “alisema Dkt. Ngaile”
Kwa kumalizia Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha udhibiti na kinga ya mionzi Bw. Machibya matulanya alitoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Prof. Ladislaus Mnyone, Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa ufunguzi rasmi wa mafunzo na viongozi wote wa TAEC kwa kufanikisha maandalizi ya semina hiyo muhimu huku akiwashukuru wanahabari kwa muitikio wa kushiriki semina hiyo muhimu.