Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imetoa mafunzo ya msingi ya siku mbili ya matumizi salama ya vyanzo vya mionzi kwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya vyanzo vya mionzi na usalama wake kwa watumishi hao.
Aidha, mafunzo hayo pia yalilenga kutoa elimu ya usalama wa wafanyakazi wanaotumia vyanzo hivyo vya mionzi.
Mafunzo hayo yalitolewa kiwandani hapo kwa wafanyakazi watano ambao ni wahandisi na wanasayansi wa Dangote.
Mtafiti na Mkuu wa Kituo cha TAEC Mkoa wa Mtwara, Bw. Machibya Matulanya, alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya majukumu ya tume ambayo yapo kwa mujibu wa Kifungu cha 6(1)(o) cha Sheria ya Nguvu za Atomiki Na. 7 ya mwaka 2003.
Alisema mafunzo hayo yalifanyika katika muda mwafaka wakati ambapo viongozi wa mataifa karibu yote duniani wanasisitiza usalama wa vyanzo vya mionzi pamoja na kulinda watumiaji.
Mafunzo hayo yataleta tija kubwa kwa wafanyakazi wa kiwanda cha Dangote kwani yatawawezesha kutumia vyanzo vya mionzi pamoja na kufuata sheria za matumizi salama ya mionzi nchini, alisema Matulanya.
Aidha, TAEC itaendelea kutoa mafunzo zaidi ya namna hiyo kwenye viwanda mbalimbali hapa nchini vinavyotumia vyanzo vya mionzi kwa lengo la kuhakikisha watumiaji wanakuwa salama.