Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) na Jeshi la Polisi leo Juni 10, 2022 wamesaini muendelezo wa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa ulinzi na usalama wa vyanzo vya mionzi hapa nchini.
Makubaliano hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Jeshi la Polisi linatoa ulinzi wakati wa usafirishaji wa vyanzo vya mionzi pamoja na kuhakikisha ulinzi wa vituo vinavyofungiwa kutumia vyanzo vya mionzi kutokana na sababu za ukiukwaji wa sheria na taratibu za matumizi salama ya mionzi hapa nchini.
Lengo kuu ni kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa vyanzo vya mionzi nchini na kuepusha vyanzo hivyo kuangukia kwenye mikono isiyo salama na kutumika vibaya katika matukio ya kihalifu/kigaidi na kuleta taharuki katika jamii
Makubaliano haya yametiwa saini na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi Ndugu Liberatus Sabas aliyekuwa ameambatana na viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi SACP Justus Kamugisha, ACP Marisone Mwakyoma na ACP Mary Kipesha kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini.
Kwa upande wa TAEC mkataba huo ulisainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Dkt. Justine Ngaile aliyekuwa akimuwakilisha Profesa Lazaro Busagala, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania