Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) inashiriki kwenye maonesho ya Wakulima maarufu kama NANE NANE yanayofanyika kitaifa mkoa wa Simiyu katika viwanja vya Nyakabindi na katika mkoa wa Arusha kweye viwanja vya Taso.
Ufunguzi wa maonesho hayo kitaifa umefanyika tarehe moja Agosti Mkoani Simiyu ambapo Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan ndie alikuwa mgeni rasmi wa maonesho ambayo yanawashirikisha Wakulima,Wajasiriamali,Taasisi mbali mbali za seikali na za binafsi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Bw. Peter Ngamilo ameleza kuwa TAEC inatoa elimu kwa wananchi wanaohudhuria maonesho hayo juu ya masuala mbali mbali ikiwemo jinsi gani Teknolojia ya Nyuklia inavyotumika katika sekta mbali mbali hapa nchini.
Bw. Ngamilo amesema kuwa Teknolojia ya Nyuklia inatumika katika sekta ya Maji, Mifugo, Kilimo, Viwanda na Uchimbaji wa Madini na Afya, hivyo ni fursa ya pekee kuweza kuhudhuria katika Viwanja hivyo ili kupata elimu juu ya matumizi ya Teknolojia ya Nyuklia hapa nchini.
Maonesho hayo yanatarajiwa kufungwa kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli tarehe 8/8/2020. Kauli mbiu ya maonesho hayo kwa mwaka huu ni “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020“.