Ufadhili wa masomo kupitia Mh. Mama Samia kwa wanafunzi wa ndani kufanya masomo ya teknolojia ya nyuklia nje ya nchi

May 29, 2024

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda amezindua mpango maalum wa Kitaifa wa ufadhili wa masomo kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa ndani kufanya masomo ya teknolojia ya nyuklia nje ya nchi.

Ufadhili huo uliozinduliwa ni kuongeza wigo wa ufadhiri wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, na ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuongeza utendaji wa sekta ya teknolojia ya nyuklia nchini Tanzania.

Mpango huo utakaoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Tume ya Nguvu za AtomuTanzania (TAEC), utawawezesha wanafunzi wahitimu wa kidato cha sita, hasa wale wenye ufaulu mzuri kwenye masomo ya sayansi kusoma masomo ya teknolojia ya nyuklia katika vyuo vikuu vinavyotambulika duniani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo wa kusaidia, Prof. Mkenda alibainisha kuwa mbali na kuwahamasisha wanafunzi wa ndani kufanya masomo ya sayansi na teknolojia, mpango uliozinduliwa unalenga kuziba pengo lililopo la idadi ya wataalam wa teknolojia ya nyuklia nchini Tanzania.

“Teknolojia ya nyuklia ni miongoni mwa sekta nyeti katika kukuza sekta ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania, hivyo programu hii ni kwa ajili ya kuruhusu nchi kuzalisha idadi ya kutosha ya wataalam wa hali ya juu na wenye ujuzi wa kushughulikia sekta hii ili kuleta maendeleo yanayohitajika. ”  alisema.

Prof. Mkenda alitoa changamoto kwa wanafunzi wa sayansi nchini Tanzania kuhakikisha wanafanya vyema katika masomo yao ya kila siku ili kupata fursa ya kunyakua ufadhili huo muhimu.

Pia alibainisha kuwa, teknolojia ya nyuklia inatumika duniani kote kusaidia maendeleo ya sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na afya, madini, ujenzi na uzalishaji wa nishati ya umeme, akisema Serikali imedhamiria kutekeleza mipango kadhaa wa kuendeleza utendaji wa sekta hiyo muhimu. .

Mwaka jana, Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ilianza mpango muhimu wa kufadhili kila mwaka angalau wanafunzi watano bora wa sayansi kuendelea na masomo ya teknolojia ya nyuklia nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TAEC (DG) Prof. Lazaro Busagala, amesema mpango huo utakaogharimu hadi shilingi bilioni 2.6/- utadumu kwa miaka mitatu mfululizo, kwa lengo la kukuza ubunifu katika nyanja mbalimbali za sayansi nchini kote.

“Programu hiyo pia inalenga kuvutia na kuhamasisha wasichana wengi zaidi kufanya masomo ya sayansi, kuanzia ngazi ya sekondari hadi elimu ya juu,” alisema na kuongeza hatua hiyo pia inaendana na Ilani ya Chama tawala (Chama Cha Mapinduzi).

Mbali na wale watakaofadhiliwa kwa masomo zaidi nje ya nchi, wanafunzi wengine waliofaulu vizuri katika masomo ya sayansi watasaidiwa kuboresha zaidi masomo yao katika vyuo mbalimbali vya ndani.

Hifadhi za nyaraka