Kwa mara nyingine Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania imeshiriki kikamilifu maonesho ya 44 ya kimataifa ya biashara na kutoa elimu juu ya majukumu ya udhibiti wa mionzi na uhamasishaji wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.
Maonyesho haya ya siku kumi na tatu (13) yalizinduliwa na Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 26 Juni, 2020, na yalianza rasmi mnamo tarehe 1 Julai, 2020, na kuhitimishwa rasmi tarehe 13 Julai, 2020 na Mhe. Amina Salum Ally, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika kipindi chote cha maonesho jumla ya watembeleaji 300 walifika bandani na kujipatia elimu juu ya kazi mbalimbali za udhiti wa mionzi na uhamasishaji wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini. Katika maonesho haya TAEC ilitoa majibu ya maswali yaliyoulizwa juu ya sababu za msingi za upimaji wa mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa kama vile usafirirshaji holela wa vyanzo vya mionzi (illicit trafficking), viasili vya mionzi kwenye mazingira yetu kutokana na ukweli kwamba nchi yetu ina madini ya urani katika maeneo mbalimbali nchini hivyo kupelekea kupima mionzi katika mnyororo wa bidhaa,.
Pia watembeleaji walijulishwa kuwa TAEC ni taasisi iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria kama ilivyoainishwa katika Sheria Namba 7, ya mwaka 2003 na kupewa majukumu ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi ili kulinda wagonjwa, wafanyakazi na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi .
Watembeleaji wamefurahishwa na namna elimu ilivyotolewa kwa njia mbalimba zikiwemo video fupi, vipeperushi, vijarida, na maelezo kutoka kwa watumishi walioshiriki maonesho hayo ambao ni Bw. Alex Muhulo ambaye ni mtafiti mwandamizi, Bw. Vitus Abel ambaye ni mtafiti wa sayansi ya nyuklia na Bw. Peter Ngamilo ambaye ni Afisa Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume.
Watembeleaji walielezwa ya kuwa matumizi ya mionzi nchini yako katika sekta mbalimbali kama vile afya, mifugo, kilimo, ujenzi, utafiti na maji, Hivyo TAEC ikiwa ndio taasisi pekee iliyopewa mamlaka kisheria ina jukumu kubwa la kuakikisha watumiaji wa mionzi katika hizo sekta na watanzania kwa ujumla wake wanakuwa salama dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi
Vile vile watembeleaji walijulishwa kuwa TAEC iko mbioni kuanza kutumia teknolojia ya nyuklia katika uhifadhi wa vyakula, mazao ili kuziongezea muda wa matumizi na kuzikinga dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na vimelea vya vijidudu ambapo kwa kutumia teknolojia hii kutaboresha bidhaa za viwandani na vifaa vya matibabu.