Wafanyakazi wa TAEC Wanolewa Vita Dhidi ya Rushwa Sehemu za Kazi

Feb 17, 2021

Wafanyakazi wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) wameshiriki semina ya siku moja  ya utawala bora na mbinu  za kupambana na rushwa mahala pa kazi, Jumanne, 16 Februari 2021.

Semina hiyo imeendeshwa na Tasasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ofisi ya Arusha.

Lengo la semina hiyo ni kuwapa wafanyakazi wa TAEC uelewa katika kupambana na masuala ya rushwa katika sehemu zao za kazi na kuboresha utendaji wao.

Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Lazaro S. P. Busagala akifungua semina hiyo amesema kupiga vita rushwa ni jambo muhimu sana katika nchi na kuomba wafanyakazi wote kuhakikisha wanajitahidi kufanya kazi kwa kufuata Sheria, taratibu na miongozo sehemu ya kazi.

“Tukitekeleza kazi kwa kujiepusha na rushwa tutaona maendeleo yanakuja katika taasisi yetu na katika Nchi kwa ujumla, hivyo nawaomba wafanyakazi wenzangu tusipokee wala kutoa rushwa wala kutengeneza njia za kupata rushwa” alisema Prof. Busagala.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu amewapongeza wafanyakazi wa TAE kwa kuendelea kuwa waadilifu katika kazi zao.

Prof. Busagala alibainisha kuwa katika ukaguzi uliofanyika katika miaka miwili iliyopita, utendaji wa wafanyakazi wa TAEC haujabainisha uwepo wa rushwa na kuwaomba wafanyakazi kutenda haki na kuhakikisha rushwa inatokomezwa katika maeneo wanayofanyia kazi.

Mtoa mada katika semina hiyo, Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU Kanda ya Kaskazini, Bi. Frolence Mwita amesema rushwa imekuwa ikiathiri sana dunia nzima lakini, hata hivyo, TAKUKURU imeweka mikakati ya kupambana na tatizo hilo.

Amewaomba wafanyakazi wa TAEC kuepuka vitendo vya rushwa katika sehemu zao za kazi kwani rushwa inadhoofisha utendaji mzima wa uletaji maendeleo ya kiuchumi nchini.

Hifadhi za nyaraka