Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania

"Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa"
Nyumbani / Habari / TAEC YASISITIZA UMUHIMU WA KUINGIZA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA KATIKA MTAALA WA ELIMU YA MSINGI

TAEC YASISITIZA UMUHIMU WA KUINGIZA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA KATIKA MTAALA WA ELIMU YA MSINGI

TAEC YASISITIZA UMUHIMU WA KUINGIZA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA KATIKA MTAALA WA ELIMU YA MSINGI

Published on July 10, 2025

Article cover image

Kigali, Rwanda

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Prof. Najat Kassim Mohamed, ameshauri kwamba somo linalohusu teknolojia ya nyuklia liingizwe katika mitaala ya elimu kuanzia ngazi ya chini, ili kuwaandaa vijana wanaoweza kushiriki kikamilifu katika kazi zinazohusisha matumizi ya teknolojia hiyo muhimu.

Prof. Najat alitoa rai hiyo wakati akichangia hoja katika Mkutano wa Afrika kuhusu Masuala ya Teknolojia ya Nyuklia, uliofanyika jijini Kigali, nchini Rwanda. Alisisitiza kuwa kuanzisha elimu ya nyuklia mapema kutasaidia kuijenga Tanzania yenye wataalamu wa ndani watakaotumika katika sekta mbalimbali zinazohusiana na matumizi salama na ya kisasa ya teknolojia ya nyuklia.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, alisema kuwa Tanzania inatarajia kuanza kuzalisha umeme wa nyuklia na kuuongeza katika Gridi ya Taifa kama njia ya kukabiliana na mahitaji makubwa ya umeme yanayosababishwa na ongezeko la viwanda nchini.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeiagiza Wizara ya Nishati chini ya uongozi wangu kuhakikisha kwamba hivi karibuni umeme utakayozalishwa unajumuishwa katika Gridi ya Taifa,” alisema Dk. Biteko.

Aliongeza kuwa, serikali imekuwa ikitekeleza jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa mikakati ya pamoja ya taasisi za serikali ili kufanikisha azma hiyo. Aidha, alibainisha kuwa uzalishaji wa umeme wa nyuklia ni wa gharama nafuu na rafiki kwa mazingira, tofauti na baadhi ya vyanzo vingine vya nishati.

Miongoni mwa jitihada hizo, Dk. Biteko alitaja kuwa mwezi Juni 2025, Serikali ya Tanzania iliandaa warsha kwa wadau wa sekta ya nyuklia pamoja na hatua ya kuanzisha taasisi maalum ya kuratibu na kusimamia shughuli za nyuklia nchini.

 “Serikali yangu itahakikisha inaendeleza mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa nishati kwa kutumia nyuklia kwa kutunga sera thabiti na kuanzisha mifumo ya sheria na udhibiti kwa ajili ya usimamizi wa raslimali ya nyuklia na uzalishaji wa umeme unaotokana na nyuklia,” alisisitiza Dk. Biteko.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazochukua hatua madhubuti za kuhakikisha teknolojia ya nyuklia inatumika kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na sekta za afya, kilimo, viwanda na nishati.