Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania

"Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa"
Nyumbani / Habari / TAEC YASHIRIKI MKUTANO MKUU WA 70 WA IAEA NCHINI AUSTRIA

TAEC YASHIRIKI MKUTANO MKUU WA 70 WA IAEA NCHINI AUSTRIA

TAEC YASHIRIKI MKUTANO MKUU WA 70 WA IAEA NCHINI AUSTRIA

Published on September 28, 2026

Article cover image

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeshiriki katika Mkutano Mkuu wa 70 wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), uliofanyika Vienna, Austria, kuanzia tarehe 14 hadi 18 Septemba 2026.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo; Balozi wa Tanzania nchini Austria, Naimi Sweetie Hamza Aziz; Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat Kassim Mohammed; pamoja na viongozi na wataalamu wengine kutoka Tanzania.

Mkutano huo uliipa Tanzania fursa ya kushiriki katika mijadala na mikutano mbalimbali iliyolenga kuimarisha ushirikiano na IAEA katika matumizi salama na ya amani ya sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pembezoni mwa mkutano huo, ujumbe wa Tanzania ulishiriki hafla ya ufunguzi wa banda la Women in Nuclear Global (WiN Global), ambapo Mhe. Prof. Mkenda pamoja na viongozi wengine walisisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanawake na kuwajengea uwezo wa kushika nafasi za uongozi katika sekta ya nyuklia.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat Kassim Mohammed, alifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa taasisi inayosimamia masuala ya atomiki nchini Pakistan, ambapo pande hizo zilikubaliana kufufua na kuimarisha ushirikiano uliokuwepo baina yao.

Mazungumzo hayo yalijikita katika kukamilisha taratibu za Hati ya Makubaliano (MoU) ambayo mchakato wake ulikuwa haujakamilika tangu mwaka 2021. Kukamilika kwa makubaliano hayo kunatarajiwa kuweka msingi wa kuendeleza ushirikiano na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ya matumizi ya amani ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.

Ushiriki wa TAEC katika Mkutano Mkuu huo ni sehemu ya juhudi za Tanzania za kuendelea kujenga na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika matumizi salama na ya amani ya teknolojia ya nyuklia kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa.

slot gacor