IAEA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA UDSM
Published on February 13, 2026
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi kwa Afrika kutoka Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu Duniani (IAEA) Bwana Gashaw Gebeyehu Wolde amesema IAEA itaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika kuhakikisha kozi mbili mpya za Shahada ya Sayansi katika Fizikia Tiba na Shahada ya Umahiri ya Sayansi katika Fizikia Tiba zinafanikiwa kutoa wahitimu bora watakaosaidia kutoa huduma katika hospitali mbalimbali nchini.
Wolde ameyasema hayo alipotembelea Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kufanya kikao Pamoja na uongozi wa Chuo hicho na kupata taarifa ya namna kozi hizo zinavyoendelea ambapo IAEA imeahidi kusaidia kutoa vifaa kwa ajili ya kujifunzia saambamba na kuimarisha maabara ya fizikia ili iweze kusaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Kozi za Shahada ya Sayansi katika Fizikia Tiba na Shahada ya Umahiri ya Sayansi katika Fizikia Tiba zilikuwa zinatolewa nchini Ghana na Afrika Kusini pekee kwa upande wa bara la Afrika ambapo IAEA ilisaidia kuanzishwa kwa kozi hizo katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambapo wanafunzi watasoma mwaka mmoja na mwaka mwingine watafanya mazoezi kwa vitendo katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es salaam upande wa Taalum Prof. Rose Upor amesema kutokana na umuhimu wa kozi hizo zinazotolewa sasa hivi Chuo kikuu cha Dar es salaam kimeamua wanafunzi watakaotoka katika ukanda wa nchi za SADC waweze kulipa ada saw ana wanafunzi wa kitanzania ili kusaidiana kukabiliana na upungufu wa wataalamu wa eneo hilo ambao wanahitajika kwa wingi.
Aidha Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania Prof. Najat Kassim Mohammed amesema ziara ya viongozi wa IAEA ni kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu sambamba na kutembelea miradi inayofadhiliwa na IAEA ili kuona namna ya kuiimarisha zaidi.