TAEC YAENDELEA KUWA KITOVU CHA ELIMU YA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA SABASABA 2026
Published on July 03, 2026
Dar es Salaam.
Leo ikiwa ni siku ya tano tangu kuanza kwa ushiriki wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA 2026), wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wameendelea kufurika katika banda la TAEC lililopo Banda Kubwa la Jakaya Kikwete, Vyumba Na. 60 na 61, kujionea na kujifunza namna teknolojia ya nyuklia inavyochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
TAEC inaendelea kutumia maonesho haya kama jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi, wadau na wawekezaji kwa kutoa elimu kuhusu majukumu yake ya kisheria ya kusimamia matumizi salama na ya amani ya teknolojia ya nyuklia pamoja na mionzi, sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia hiyo katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Katika siku hizi tano za maonesho, mamia ya wananchi, wanafunzi, watafiti, wataalamu, wafanyabiashara na wageni kutoka ndani na nje ya nchi wametembelea banda la TAEC na kupata ufahamu wa kina kuhusu mchango wa teknolojia ya nyuklia katika kuboresha maisha ya Watanzania.
Wataalamu wa TAEC wamekuwa wakitoa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika sekta ya afya kupitia uchunguzi na tiba ya magonjwa mbalimbali, hususan saratani; sekta ya kilimo kupitia uboreshaji wa mbegu, udhibiti wa visumbufu vya mazao na kuongeza uzalishaji; sekta ya mifugo kupitia udhibiti wa magonjwa na kuboresha uzalishaji; sekta ya viwanda kupitia vipimo visivyoharibu bidhaa (Non-Destructive Testing), pamoja na matumizi katika utafiti wa kisayansi, usimamizi wa mazingira na rasilimali za maji.
Aidha, wananchi wameendelea kupata elimu kuhusu jukumu la TAEC katika kusimamia usalama wa vyanzo vya mionzi nchini ili kuhakikisha matumizi yake yanakuwa salama kwa wafanyakazi, wagonjwa, jamii na mazingira, kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vya kimataifa.
Miongoni mwa vivutio vikubwa katika banda la TAEC ni maonesho ya vifaa mbalimbali vinavyotumika katika usimamizi wa mionzi, machapisho ya elimu kwa umma, pamoja na maelezo ya wataalamu yanayoondoa dhana potofu kuhusu teknolojia ya nyuklia na kueleza manufaa yake katika maendeleo ya taifa.
Wananchi wengi waliotembelea banda hilo wameeleza kufurahishwa na elimu wanayoipata, wakibainisha kuwa imewasaidia kuelewa kwa undani nafasi ya teknolojia ya nyuklia katika kuboresha huduma za afya, kuongeza uzalishaji wa kilimo na mifugo, kusaidia maendeleo ya viwanda, kulinda mazingira na kuimarisha utafiti wa kisayansi.
Ushiriki wa TAEC katika maonesho haya unaendana na kaulimbiu yake ya “Nuclear Technology for Trade and Economic Development in Tanzania,” inayosisitiza mchango wa teknolojia ya nyuklia katika kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo endelevu ya uchumi wa Taifa.
TAEC inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda lake lililopo Banda Kubwa la Jakaya Kikwete, Vyumba Na. 60 na 61, katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam, ili kujionea maonesho hayo na kupata elimu ya bure kutoka kwa wataalamu kuhusu matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia na mchango wake katika sekta za afya, kilimo, mifugo, viwanda, utafiti, nishati na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Maonesho ya SABASABA 2026 yanaendelea hadi tarehe 13 Julai 2026, yakileta pamoja maelfu ya washiriki kutoka Tanzania na nchi mbalimbali duniani katika kuonesha bidhaa, huduma, teknolojia na fursa za biashara na uwekezaji. TAEC inaamini kuwa kupitia maonesho haya, wananchi wataendelea kupata uelewa sahihi kuhusu nafasi ya teknolojia ya nyuklia katika kujenga Tanzania yenye uchumi imara na maendeleo endelevu.