Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania

"Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa"
Nyumbani / Habari / Ushiriki wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Katika Mkutano wa Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia Barani Afrika (NEISA 2026), Kigali – Rwanda

Ushiriki wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Katika Mkutano wa Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia Barani Afrika (NEISA 2026), Kigali – Rwanda

Ushiriki wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Katika Mkutano wa Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia Barani Afrika (NEISA 2026), Kigali – Rwanda

Published on May 21, 2026

Article cover image

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia Barani Afrika (NEISA 2026) umefanyika Kigali, Rwanda tarehe 19 Mei 2026, ukihusisha viongozi wa kitaifa, wataalamu wa nishati, wawekezaji na mashirika ya kimataifa. Lengo kuu la mkutano huu ni kujadili namna bora ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme barani Afrika, kupunguza uchafuzi wa mazingira, kusaidia maendeleo ya viwanda, kukuza ubunifu wa teknolojia za nyuklia na kuvutia uwekezaji katika miradi ya nishati ili kuimarisha uchumi endelevu.

Ushiriki wa Tanzania

Katika mkutano huo, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alieleza kuwa Tanzania inaendelea kutathmini matumizi ya nishati ya nyuklia kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuongeza vyanzo vya nishati. Alisisitiza kuwa teknolojia mpya kama Small Modular Reactors (SMRs) na Micro Modular Reactors (MMRs) zinaweza kuwa suluhisho sahihi kwa nchi zinazoendelea.

Aidha, Rais Dkt. Samia alibainisha maeneo matatu muhimu kwa ukuaji wa sayansi na teknolojia ya nyuklia:

  • Mifumo imara ya udhibiti
  • Wataalamu wenye ujuzi
  • Usimamizi madhubuti wa usalama na kuzingatia viwango vya kimataifa

Aliongeza kuwa ili kuimarisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika uzalishaji wa nishati, ni lazima kuzingatia masuala ya upatikanaji wa fedha, maandalizi ya mifumo ya udhibiti, uwezo wa taasisi, uelewa wa wananchi pamoja na ushirikiano wa kikanda.

Ushiriki wa TAEC

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Profesa Najat Kassim Mohammed, alihudhuria mkutano huo akiambatana na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia na Huduma za Ufundi, Dkt. Remigius Kawala.

Profesa Najat alipata fursa ya kualikwa na Mheshimiwa Rais katika kikao cha ndani ambapo alitoa ufafanuzi juu ya maendeleo ya nyuklia nchini Tanzania. Alieleza miradi inayotekelezwa na TAEC pamoja na mipango ya kimkakati ya Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA), ikiwemo:

  • Rays of Hope – mpango wa kuimarisha uchunguzi na matibabu ya saratani nchini.
  • Atoms4Food – mpango wa kuimarisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika kilimo.
  • Ushiriki wa TAEC katika mpango wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa uzalishaji wa umeme.

Kwa nafasi yake, Profesa Najat alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kuwekeza katika utafiti, usalama na mafunzo ya wataalamu ili kuhakikisha matumizi salama na endelevu ya teknolojia ya nyuklia.

Ushiriki wa TAEC ulionyesha dhamira ya Tanzania ya kuendelea na matumizi salama ya teknolojia za kisasa za nyuklia katika sekta mbalimbali kama afya, kilimo, utafiti wa madini,viwanda na uzalishaji wa nishati.

TAEC ilipata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kuhusu masuala ya usalama wa nyuklia, maandalizi ya mifumo ya udhibiti wa teknolojia za nyuklia, pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya nishati. Tanzania inaendelea kukuza matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya matumizi salama na ya amani kupitia sera na sheria zinazosimamiwa na TAEC.

Aidha, ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo uliendana na maono ya serikali ya kukuza sekta ya nishati na kuimarisha ushirikiano wa kikanda ndani ya Afrika Mashariki. Katika mkutano huo viongozi mbalimbali wa Afrika walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kuendeleza miradi ya nyuklia, kuongeza uwekezaji na kujenda uwezo wa wataalamu wa ndani.

Kwa ujumla, ushiriki wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) katika mkutano huo wa NEISA 2026 uliiwezesha Tanzania kuendelea kujijengea nafasi katika mjadala wa kimataifa kuhusu mustakabali wa nishati ya nyuklia barana Afrika. Mkutano huo pia uliweka misingi ya ushirikiano mpya wa kitaalamu, kiteknolojia na kiuchumi ambao unaweza kusaidia Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo endelevu katika miaka ijayo.

Mkutano wa NEISA 2026  uliandaliwa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo Wakala wa  Nguvu za Atomu Duniani (IAEA), United Nationa Economic Commission for Africa. World Nuclear Association pamoja na Rwanda Atomic Energy Board. Ushirikiano huu uliifanya NEISA kuwa jukwaa muhimu kwa nchi za Afrika kujifunza uzoefu wa kimataifa kuhusu uendelezaji wa nishati ya nyuklia na teknolojia za  Small Modular Reactors (SMRs)

  1. Mashirika haya yamechangia kwa kutoa utaalamu, kuwezesha miradi ya mafunzo, na kuunga mkono mipango ya Afrika ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu.

slot gacor