Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania

"Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa"
Nyumbani / Habari / SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAENDELEA KUKUZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA KWA MAENDELEO YA TAIFA

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAENDELEA KUKUZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA KWA MAENDELEO YA TAIFA

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAENDELEA KUKUZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA KWA MAENDELEO YA TAIFA

Published on February 06, 2026

Article cover image

TAEC Yaimarisha Ushirikiano na IAEA Kuongeza Tija katika Afya, Kilimo na Usalama wa Chakula

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kukuza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu, hatua inayochochea maendeleo ya matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Profesa Najat Kassim Mohammed, wakati wa ziara ya ujumbe wa wataalamu kutoka Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomiki (IAEA) wenye makao makuu Vienna, Austria, waliotembelea Ofisi za TAEC zilizopo Njiro, jijini Arusha.

Profesa Najat alisema ujio wa ujumbe huo ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na IAEA katika kuhakikisha matumizi salama, yenye tija na endelevu ya teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Alieleza kuwa ziara hiyo imelenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nyuklia inayotekelezwa nchini kwa kushirikiana na IAEA pamoja na kubaini maeneo mapya ya ushirikiano yatakayosaidia kuendeleza matumizi ya teknolojia hiyo.

Aidha, Profesa Najat alibainisha kuwa mafanikio yanayopatikana katika utekelezaji wa miradi hiyo yanatokana na maono na msukumo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayosisitiza matumizi ya sayansi na teknolojia kama nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya Taifa. Aliongeza kuwa kupitia uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeendelea kupanua wigo wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika sekta za afya, kilimo, usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumzia sekta ya afya, Profesa Najat alisema teknolojia ya nyuklia imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za uchunguzi na tiba ya saratani pamoja na kuimarisha huduma za tiba ya mionzi katika hospitali mbalimbali nchini. Alisema juhudi hizo zinaendana na mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

Katika sekta ya kilimo, alieleza kuwa matumizi ya teknolojia ya nyuklia yamechangia kuboresha uzalishaji wa mazao, kudhibiti visumbufu wa mazao na kuimarisha uhifadhi wa chakula kwa kutumia mbinu za kisasa zinazosaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna. Alisisitiza kuwa hatua hizo zinaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa wananchi wanaotegemea kilimo.

Profesa Najat pia alisisitiza kuwa TAEC inaendelea kusimamia na kuimarisha mifumo ya usalama na ulinzi wa mionzi ili kuhakikisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia yanafanyika kwa kuzingatia viwango na miongozo ya kimataifa inayotolewa na IAEA. Alieleza kuwa usalama wa binadamu, mazingira na mali unaendelea kuwa kipaumbele kikuu katika utekelezaji wa shughuli zote zinazohusisha matumizi ya mionzi nchini.

Kwa upande wake, ujumbe wa IAEA ulipongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia TAEC katika kusimamia na kuendeleza matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia. Ujumbe huo ulieleza utayari wa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kujenga uwezo wa wataalamu, kuimarisha miundombinu pamoja na kusaidia utekelezaji wa miradi mipya yenye manufaa kwa wananchi.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kuhakikisha teknolojia ya nyuklia inatumika kwa madhumuni ya amani na maendeleo endelevu, sambamba na kuimarisha usalama wa matumizi ya teknolojia hiyo katika nchi wanachama wa IAEA.

TAEC itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha teknolojia ya nyuklia inachangia kikamilifu katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Taifa na utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi shindani unaotegemea sayansi, teknolojia na ubunifu.