TAEC Yaendesha Mafunzo ya Usalama wa Mionzi kwa Watumiaji wa Vifaa vya Ukaguzi wa Mizigo (Baggage Scanners) Jijini Arusha
Published on October 08, 2025

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeanza rasmi mafunzo ya kitaifa kuhusu usalama wa mionzi kwa watumiaji wa vifaa vya ukaguzi wa mizigo (baggage scanners), yakifanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 6 hadi 10 Oktoba 2025. Mafunzo haya yanalenga kuimarisha uelewa wa matumizi salama ya teknolojia ya mionzi katika taasisi zinazohusika na usalama wa abiria na mizigo.
Mafunzo hayo yamewaleta pamoja washiriki 31 kutoka taasisi mbalimbali, ambapo 28 wanatoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), mmoja kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mmoja kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na mwingine kutoka kampuni ya usambazaji wa vifaa vya ukaguzi wa mizigo (baggage scanners). Washiriki hao wanapata mafunzo ya nadharia na vitendo kuhusu uendeshaji salama wa vifaa vya mionzi, udhibiti wa mionzi, na hatua za dharura katika mazingira ya kazi.