TAEC yashiriki Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Dodoma
Published on July 03, 2026
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeanza rasmi kushiriki maonesho ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma kuanzia tarehe 16 Juni 2026. Maonesho haya yameanza leo na yanatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 23 Juni 2026.
TAEC inashiriki ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya kisheria katika udhibiti wa matumizi salama ya mionzi ili kulinda mazingira, wagonjwa, wafanyakazi na wananchi dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi. Vilevile, TAEC inatoa elimu juu ya uhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, mifugo, maji, nishati, viwanda, migodi pamoja na utafiti wa kisayansi.
Mbali na hayo, TAEC inatoa elimu kuhusu namna inavyotekeleza na kuwekeza kimkakati mpango wa Samia Extended Scholarship. Mpango huu ni dira ya maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuandaa wataalamu wa nyuklia watakaosimamia na kuendeleza teknolojia ya nyuklia hususan katika tiba na nishati. Kupitia mpango huu, wanafunzi bora wa masomo ya sayansi wanapatiwa udhamini kusoma katika vyuo vikuu bora duniani ili baadaye waweze kusimamia miradi ya kimkakati ya kitaifa na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.
Katika wiki hii ya maadhimisho, TAEC pia inatoa elimu juu ya ujumuishi na ubunifu unaotekelezwa na Tanzania Young Generation in Nuclear (TYGN). Kikundi hiki kinawaunganisha vijana wenye shauku ya mageuzi kupitia teknolojia ya atomu, kikilenga kujenga mtandao wa viongozi wa baadaye katika sekta ya nishati.
Aidha, TAEC inawakaribisha wanawake kutembelea banda lake ili kupata elimu kuhusu mtandao wa kitaifa wa wanawake wanaofanya kazi au kujihusisha na sekta ya nyuklia na mionzi nchini, yaani Women in Nuclear Tanzania (WiN TZ). Jumuiya hii inalenga kuelimisha na kukuza usawa wa kijinsia katika nyanja za nyuklia, mionzi, nishati, afya na mazingira. Lengo ni kuhakikisha wanawake wanasayansi wanapata fursa sawa na kufikia uwiano wa asilimia 50 kwa 50 katika nafasi za uongozi na utafiti. WiN TZ pia inasaidia kuvunja dhana kwamba sekta ya nyuklia ni ya wanaume pekee, na kuhamasisha vijana wa kike kuingia kwenye taaluma za sayansi na teknolojia.
TAEC inawaalika wananchi wote wa Dodoma na maeneo ya jirani kutembelea banda lake katika Viwanja vya Chinangali ili kujipatia elimu muhimu kuhusu usalama wa mionzi na fursa za kitaaluma zinazotolewa kupitia miradi ya kitaifa.