Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania

"Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa"
Nyumbani / Habari / Tanzania Yaweka Mikakati ya Nishati ya Nyuklia Kupitia Warsha ya Kitaifa ya Uelewa wa Umuhimu wa NEPIO

Tanzania Yaweka Mikakati ya Nishati ya Nyuklia Kupitia Warsha ya Kitaifa ya Uelewa wa Umuhimu wa NEPIO

Tanzania Yaweka Mikakati ya Nishati ya Nyuklia Kupitia Warsha ya Kitaifa ya Uelewa wa Umuhimu wa NEPIO

Published on June 10, 2025

Article cover image

Dar es Salaam, 10 Juni 2025.
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) inaendesha warsha ya kitaifa ya Uelewa juu ya Matumizi ya Nishati ya Nyuklia na Umuhimu wa kuanzishwa kwa Taasisi ya Utekelezaji wa Mpango wa Nishati ya Nyuklia (NEPIO). Warsha hiyo inafanyika katika Hoteli ya Tiffany Diamond, na imewakutanisha wadau takribani 60 kutoka taasisi za serikali na sekta binafsi.

Profesa Joseph Msambichaka,  Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC ambaye alikuwa mgeni rasmi, alieleza umuhimu wa nishati ya nyuklia katika kukidhi mahitaji ya nishati ya muda mrefu nchini. Alihimiza ushirikiano wa kitaifa kuhakikisha mchakato huu unatekelezwa kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia maendeleo endelevu.

Katika salamu za ufunguzi, , kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesisitizwa juu ya umuhimu wa elimu na ujenzi wa uwezo katika safari ya kuelekea kwenye matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa uzalishaji wa nishati.

Naye Mhandisi Innocent Luoga, Kamishna wa Nishati Jadidifu, alielezea namna ambavyo nishati ya nyuklia inaweza kuongezea nguvu vyanzo vingine vya nishati kama vile jua na upepo, na akaeleza dhamira ya Serikali kuhakikisha mchanganyiko imara wa nishati nchini.

Katika kutoa shukrani, Profesa Najat Kassim Mohammed, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, aliwashukuru washiriki wote na wadau waliojitokeza, akiahidi kwamba TAEC iko tayari kuongoza mchakato wa kiufundi, kisheria na uhamasishaji wa umma kuelekea Tanzania yenye uwezo wa kutumia nishati ya nyuklia kwa usalama na ufanisi.

Warsha hii itaendelea kwa siku kadhaa zijazo kwa mijadala ya kitaalamu na mipango madhubuti ya kuanzisha NEPIO na kuhakikisha taifa linaingia kwenye teknolojia ya nyuklia kwa maandalizi bora.