Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania

"Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa"
Nyumbani / Habari / Ubia wa ZFDA na IAEA Kuimarisha Usalama wa Chakula Zanzibar

Ubia wa ZFDA na IAEA Kuimarisha Usalama wa Chakula Zanzibar

Ubia wa ZFDA na IAEA Kuimarisha Usalama wa Chakula Zanzibar

Published on February 13, 2026

Article cover image

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) Dkt. Burhani Othman Simai amesema ushirikiano kati ya ZFDA na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu duniani (IAEA) umesaidia kupatikana kwa vifaa vya maabara vinavyosaidia kupima kemikali za sumu kwenye chakula kama vile mabaki ya dawa za kutibu wanyama.sambamba na wataalamu wa ZFDA kupata mafunzo ndani na nje ya nchi.

Dkt. Simai ameyasema hayo baada ya kupokea ugeni kutoka Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu duniani (IAEA) ugeni ulioongozwa na Bwana Gashaw Gebeyehu Wolde, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi kwa Afrika, pamoja na Bi. Azza Kashlan, Afisa wa Usimamizi wa Programu.

Mradi wa kuimarisha usalama wa chakula kwa kujenga uwezo wa maabara ya ZFDA ni mradi wa miaka minne ambapo kwa sasa umeshamaliza miaka miwili na manufaa yaliyopatikana ni pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi wa ZFDA sambamba na upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya kupima sampuli za chakula ili kuhakisha usalama kwa watumiaji.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi kwa Afrika Bwana Gashaw Gebeyehu Wolde, amesema kuwa wanatarajia kushirikiana na ZFDA katika mradi mwingine wa kupima mabaki ya plastiki kwenye chakula ili kuhakikisha usalama.

Aidha Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania Prof. Najat Kassim Mohammed amesema lengo la ziara ya viongozi kutoka Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu duniani (IAEA) ni kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri ya muda mrefu sambamba na kutembelea miradi wanayofadhili hapa nchini.