Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) inaendesha warsha inayohusisha wataalamu wa kitaifa wa kinga na udhibiti wa mionzi kutoka katika nchi 23 kutoka katika Bara la Afrika ambao ni wanachama wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani
Lengo la warsha hii ilionza hivi leo, ni kujadiliana uzoefu wa nchi za Afrika zilizopata kutekeleza viwango vya kinga na udhibiti wa mionzi vilivyotolewa mwaka 2014 na shirika la kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani na pia kujadili changamoto zilizowahi kujitokeza na kuzifanyia marekebisho.
Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Prof. Lazaro Busagala amewataka watalaamu hao kujadiliana na kutoa mapendekezo sahihi yatakayosaidia kuwakinga wananchi na mazingira katika nchi zao dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha mionzi katika Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) Bwana Tony Colgan amesema kuwa washiriki wa mkutano huo wanapaswa kujadiliana na kupata mbinu zitakazowezesha kuboresha ulinzi na usalama katika mionzi. Amesistiza kuwa IAEA inapenda kupata mrejesho wa uzoefu wa nchi hizo katika kutumia viwango hivyo vya kimataifa.