Mafunzo Kwa Wataalamu Wa Ulinzi Na Usalama Wa Vyanzo Vya Mionzi Nchi Sita Za Afrika

Apr 3, 2019

TAARIFA KWA UMMA

2 Aprili, 2019, Arusha

Jumla ya wataalamu 25 wa Ulinzi na Usalama wa vyanzo vya mionzi kutoka katika nchi sita za Afrika wanashiriki katika mafunzo ya wiki mbili ya jinsi ya kuendesha mafunzo ya ulinzi na usalama wa vyanzo vya mionzi. Mafunzo hayo yanaendeshwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kwa ushirikiano na Jumuia ya Umoja wa Ulaya (EU).

Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwapatia ujuzi wakufunzi hawa namna ya kufundisha wataalamu mbalimbali wanaohusika na usalama wa vyanzo vya mionzi katika nchi zao. Mafunzo haya yaliyoanza jana tarehe 01 Aprili, 2019 katika ofisi za Makao makuu ya Tume, Jijini Arusha, yanatarajiwa kufika kilele siku ya ijumaa tarehe 12 Aprili, 2019

Matarajio ya mafunzo haya kwa wakufunzi hawa wa usalama wa vyanzo vya mionzi ni kuongeza uwezo na kuwa na nafasi ya kuongoza kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kitaifa katika nchi zao ili kuhakikisha kuwa vyanzo vya mionzi vinatumika katika njia zilizo salama na halali.

Washiriki hawa kutoka katika idara za Polisi, Walinzi waliopo katika mipaka na wasimamizi wa Tekinolojia ya Nyuklia , maafisa forodha na wataalamu wa kupambana na majanga ya nyuklia kutoka katika nchi za Burundi, Uganda, Congo (DRC), Zambia, Ghana na wenyeji Tanzania pia watafundishwa namna ya kubaini usafirishaji haramu wa vyanzo vya mionzi

Vyanzo vya mionzi visipodhibitiwa vinaweza kutumika katika vitendo vya kigaidi na kuleta madhara makubwa kwa jamii na kuathiri shughuli za kimaendeleo na kiuchumi

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania.

PICHA : Wataalamu 25 wa Ulinzi na Usalama wa vyanzo vya mionzi kutoka katika nchi sita za Afrika wanaoshiriki katika mafunzo ya wiki mbili ya jinsi ya kuendesha mafunzo ya ulinzi na usalama wa vyanzo vya mionz katika nchi zao wakiwa katika picha ya pamoja katika Makao Makuu ya Ofisi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) Jijini Arusha. Mafunzo hayo yanaendeshwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kwa ushirikiano na Jumuia ya Umoja wa Ulaya (EU).

Hifadhi za nyaraka